Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- lifuatalo ni Darsa Fupi na Muhimu kuhusiana na: “Fadhila na siri za Tasbihat az-Zahra (a.s.) na Ayatul Kursi” kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w) na Ahlul-Bayt wake watoharifu (a.s.), hasa katika mazingira ya maombolezo ya Shahada ya Bibi Fatimah az-Zahra (a.s):
Fadhila na Siri za Tasbihat az-Zahra (a.s.) na Ayatul Kursi
1. Tasbihat az-Zahra (a.s)
Asili yake na namna alivyojifunza
Imeelezwa katika riwaya kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimfundisha binti yake mpenzi, Fatimah az-Zahra (a.s.), tasbihi hii tukufu alipomwomba amtumie mtumishi wa kumsaidia kazi za nyumbani. Mtume (s.a.w.w) akamwambia: “Ewe Fatimah! Je, nisikufundishe kitu kilicho bora kuliko mtumishi?
Unapolala, sema Allahu Akbar mara 34, Alhamdulillah mara 33, na Subhanallah mara 33; hilo ni bora kwako kuliko kuwa na mtumishi.”
(Wasā’il ash-Shī‘a, Juz. 4, uk. 1024)
Fadhila na Thawabu zake
-
Imam as-Sadiq (a.s.) amesema: “Tasbih ya Fatimah az-Zahra (a.s.) baada ya kila swala ni bora zaidi kwangu kuliko kuswali rakaa elfu moja kila siku.”
(Al-Kāfī, Juz. 2, uk. 532) -
Imam al-Baqir (a.s.) amesema: “Anayesema Tasbih ya Fatimah az-Zahra (a.s.) kisha akaomba maghfirah, atasamehewa. Ni mia moja kwa ulimi wake, lakini ni elfu moja katika mizani.”
(Tahdhīb al-Ahkām, Juz. 2, uk. 105)
Siri na Maana za Kiroho
- “Allahu Akbar” mara 34 — Huthibitisha ukuu na utukufu wa Mwenyezi Mungu, na humfundisha mja kujiepusha na majivuno na mapenzi ya dunia.
- “Alhamdulillah” mara 33 — Ni ishara ya kumshukuru Mwenyezi Mungu katika kila hali, furaha au taabu.
- “Subhanallah” mara 33 — Ni kumsafisha Mwenyezi Mungu kutokana na upungufu au kasoro yoyote, na ni wito wa kuutakasa moyo.
Tasbih hii si maneno ya ulimi tu, bali ni njia ya kiroho ya tauhidi (umoja wa Mungu), ridhaa, na kujisalimisha kwa Mola.
Kwa sababu hiyo, Maimamu (a.s.) wamesema: “Hakuna kitu bora zaidi baada ya swala ya faradhi kuliko Tasbih ya Fatimah az-Zahra (a.s.).”
2.Ayatul Kursi
Fadhila zake katika Qur’ani na Hadith
Mtume Mtukufu (s.a.w.w) amesema: “Yeyote atakayesoma Ayatul Kursi baada ya kila swala ya faradhi, hakuna kitakachomzuia kuingia Peponi isipokuwa kifo.”
(Bihār al-Anwār, Juz. 89, uk. 255)
Imam Ali (a.s.) naye amesema: “Ayatul Kursi ni Bibi wa Aya zote za Qur’an, na ndani yake imo Jina Kuu la Mwenyezi Mungu.”
(Tafsīr al-Qummī, Juz. 1, uk. 68)
Siri na Maana zake
- “Allahu la ilaha illa Huwa al-Hayyul-Qayyum” - Huthibitisha umoja na uhai wa milele wa Mwenyezi Mungu.
- “La ta’khudhuhu sinatun wala nawm” - Humuondolea Mwenyezi Mungu udhaifu, uchovu au usingizi.
- “Wasi‘a kursiyyuhus-samawati wal-ardh” - Huthibitisha wigo wa elimu, mamlaka, na utawala wa Mwenyezi Mungu juu ya kila kitu.
Ayatul Kursi ni ngome ya usalama wa kiroho, kinga dhidi ya maovu, na chanzo cha nuru ya ndani ya moyo.
3. Uhusiano kati ya Tasbihat az-Zahra (a.s.) na Ayatul Kursi
- Zote mbili zinaunganisha mja na Mwenyezi Mungu kwa dhikr (ukumbusho) na tauhidi.
- Kuzisoma baada ya swala, au katika majlisi za maombolezo ya Bibi Fatimah az-Zahra (a.s.), humaanisha kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kupata utulivu wa kiroho kama alivyokuwa mama huyu mtakatifu - mfano wa subira, imani, na unyenyekevu.
Your Comment